MUUNGANO WA JUBILEE NA ODM WATILIWA SHAKA POKOT MAGHARIBI.


Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa nchini kufuatia hatua ya chama cha jubilee na kile cha ODM kutangaza mipango ya kuunda muungano kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Baadhi ya wakazi wa makutano kaunti hii ya pokot magharibi wamepuuzilia mbali muungano huo wakidai kuwa hautadumu, hasa ikizingatiwa historia ya uhusiano wa vinara wa vyama hivyo rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa ODM Raila Odinga na viongozi wengine ambao wamewahi kufanya kazi nao.
Aidha kulingana na wakazi hao muungano wa vyama vya Jubilee na ODM hautaathiri kwa vyovyote chama cha UDA ambacho kinahusishwa na naibu rais William Ruto na badala yake utatoa nafasi bora kwa chama hicho kunawiri hata zaidi.
Wakati uo huo baadhi ya wakazi wamesema kuwa muungano wa vyama hivyo unatumika kuendeleza ajenda za vinara wake rais Kenyatta na Raila kupitia mchakato mzima wa BBI kwa kile wamedai ni kwa manufaa yao ya binafsi.