BARABARA YA ATURKAN KAMATIRA YATARAJIWA KULETA MANUFAA KWA WAKAZI WA POKOT MAGHARIBI.
Ujenzi wa barabara kuu ya kutoka Aturkan mjini Kitale kaunti ya Trans nzoia hadi Kamatira kaunti hii ya Pokot magharibi ambao unanuiwa kutekelezwa na mamlaka ya barabara kuu nchini KeNHA utaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa kaunti hii hasa wafanyibiashara.
Haya ni kulingana na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye aidha amesema kuwa huenda barabara hiyo ikaimarisha hadhi ya mji wa makutano na hata kuwa na jiji kuu katika kaunti hii ya Pokot magharibi iwapo kutakuwa na mipangilio madhubuti.
Aidha Moroto amewataka wakazi ambao watakuwa karibu na barabara hiyo kutumia hiyo nafasi hasa katika kufungua biashara kama vile mikahawa ili kunufaika kutokana na wasafiri wengi ambao watakuwa wanaitumia.
Wakati uo huo Moroto ameelezea haja ya wafanyibishara kupewa muda wa kuendeleza shughuli zao hata nyakati za usiku itakapokamilika barabara hiyo muradi wazingatie masharti ya wizara ya afya katika kukabili maambukizi ya virusi vya corona.