FAMILIA YAOMBOLEZA KIFO CHA POLISI WA UTAWALA KISHAUNET
Familia moja eneo la Kishaunet kaunti hii ya Pokot magharibi inaendelea kuomboleza kifo cha mmoja wao Clement Mnang’at ambaye alikuwa mmoja wa polisi wa utawala waliouliwa majuzi kaunti ya Mandera, baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi.
Kulingana na kakake marehemu Daniel Rotino, maisha ya mwenda zake yamekatizwa takriban wiki mbili tu baada yake kutoka nyumbani kufunga pingu za maisha, huku akitoa wito kwa serikali kutowatuma maafisa wa kdf ambao ndio mwanzo wanajiunga na kikosi hicho katika maeneo hatari.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na mjombake marehemu Philip Keneo ambaye amesema visa kama hivi vitafanya vijana wengi kuhofia kujiunga na kikosi hicho huku akitoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya kulinda usalama wa maafisa wa kdf eneo hilo.
Aidha chifu wa kata ya Kishaunet Edward Kakamoi amemwomboleza mwendsa zake akitoa wito wa subira kwa jamii yake huku akiihakikishia kuwa serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha inawapa msaada unaohitajika wakati huu.
Marehemu aliaga dunia baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi kinachoaminika kutegwa na kundi gaidi la alshabaab eneo la Banisa kaunti ya Mandera ijumaa iliyopita, huku akimwacha mjane Nancy chepoisho bila mtoto.
Mwili wake unaletwa jumanne kwa mazishi ambayo yataandaliwa jumatano nyumbani kwao Kishaunet kaunti hii ya Pokot magharibi.
Visa vya maafisa wa usalama kuuliwa vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara eneo la kaskazini mashariki ya nchi kufuatia magari yao kukanyaga vilipuzi.