SHUGHULI YA KUPIMA ARDHI ENEO LA KAPCHOK YAKASHIFIWA


Mwakilishi wadi ya Kapchok kaunti hii ya Pokot magharibi Peter Lokor amekashifu jinsi shughuli ya kubaini mpaka kati kaunti hii ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda eneo la Konyao inavyoendeshwa.
Lokor amesema kuwa maafisa ambao wanaendeleza shughuli hiyo wanatumia fursa hiyo kuwatapeli wakazi wa eneo hilo ardhi zao kupitia shughuli za kupima ardhi ili wapate hati miliki za ardhi.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki Lokor amesema kuwa shughuli hiyo inaendeshwa bila kutoa elimu kwa wakazi wa eneo hilo kuhusu umuhimu wa kugawanya ardhi akidai wakazi hao wanalazimika kutoa shilingi alfu 4,500 huku akitilia shaka nambari za ardhi wanazopewa.
Aidha Lokor amesema kuwa viongozi wa kaunti hii hawana habari kuhusu shughuli inayoendelezwa eneo hilo la konyao huku akiwataka wakazi wa eneo hilo kutokubali kutapeliwa na maafisa hao.
Hata hivyo naibu kamishina eneo la Konyao Barack Abonyo amesema shughuli hiyo ni mpango wa serikali kuwapa wakazi hati miliki za ardhi na kuwa hamna mkazi yeyote anayelazimishwa bali inatekelezwa kwa hiari ya wakazi wanaotaka stakabadhi hizo.