WAKAZI WA SIGOR WALALAMIKIA KUHANGAISHWA NA MAAFISA WA POLISI


Wakazi wa eneo la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi hasa wafanyibiashara wamelalamikia kuhangaishwa na maafisa wa polisi wanaodai kuwaitisha hongo hasa siku za soko.
Wakiongozwa na aliyekuwa diwani wa wadi ya Lomut Musa Tekelezi wakazi hao wamemshutumu vikali afisa wa kusimamia kituo cha polisi cha Sigor kwa kile wamedai kuzembea kazini na kuwaacha raia wakihangaishwa na maafisa hao.
Wametaka afisa huyo kupewa uhamisho wakisema amehudumu kwenye eneo hilo kwa muda mrefu na kuwa maafisa wa polisi wamekuwa wakichukulia suala la wakazi wengi wa eneo hilo kutoelewa kiswahili vyema kuwaibia.
Wakazi hao sasa wameitaka serikali kuingilia swala hilo wakitishia kuandaa maandamano iwapo hatua kali hazitachukuliwa kwa wahusika .
Hata hivyo , kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Pokot ya kati Barmford Suru amepuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa hakuna afisa kutoka kituo cha polisi cha Sigor ambaye amemdhulumu mtu yeyote ama kuchukua hongo na kuongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na afisa yeyote atakayepatikana akihusika uovu huo .