Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom yajumuika na wakazi wa Pokot magharibi kusherehekea miaka 25

Na Benson Aswani
Kampuni ya mawasiliano nchini Safaricom inazuru maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi kuungana na wananchi katika maadhimisho ya miaka 25 tangu kuzinduliwa hapa nchini.
Akizungumza alipoongoza sherehe hizo eneo la Kacheliba, meneja wa mauzo wa kampuni hiyo katika kaunti za Pokot magharibi na Turkana Benard Kiprop alisema kampuni hiyo imeamua kugatua sherehe hizo ili kutoa shukrani kwa wateja wake maeneo mbali mbali ya nchi kwa kuendelea kuwa waaminifu.
“Tumekuja nyumbani ili tuweze kusherehekea na wateja wetu popote walipo. Tuna box tumetembea nayo, ina zawadi kem kem kwa sababu tunajua wakati unafanya sherehe mambo ya zawadi ni kitu muhimu sana,” alisema Kiprop.
Kulingana na Kiprop wananuia kuzuru maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo kukutana na wateja wake, alhamisi wakijumuika na wakazi wa chepareria huku sherehe kubwa ikiandaliwa ijumaa mjini Makutano ambapo pia zawadi mbali mbali zinatolewa kwa wateja.
“Leo tunaelekea Chepareria. Kwa hivyo wateja wa Safaricom mnakaribishwa sana. Halafu sherehe kubwa sana ya kumalizia itakuwa mjini Makutano hapo kesho ijumaa, na tutasherekea kabisa na watu wetu wa Pokot magharibi ambao tunajua ni wateja wetu,” alisema.
Baadhi ya wateja na wakala wa Safaricom walisifia huduma za kampuni hiyo katika kurahisisha mawasiliano, japo wakipendekeza kuimarishwa zaidi huduma hizo hasa maeneo ya mashinani.
