Wadau waendeleza mikakati ya kuimarisha kilimo Pokot Magharibi

Na Emmanuel Wakoli,
Wadau mbali mbali katika kaunti ya Pokot magharibi wanaendeleza ushirikiano kwa pamoja na idara ya kilimo kaunti hiyo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwenye sekta ya kilimo.


Akizungumza baada ya kikao na wadau kwenye mkahawa mmoja mjini makutano, mkurugenzi mkuu wa shirika la Declares Jefferson Mudaki alisema mbinu ambazo mara nyingi hutumika katika kilimo zinachangia katika uharibifu wa mazingira, na kwa ushirikiano na wadau mbali mbali wanalenga kubuni mradi wa kukabili hali hiyo.


“Mara nyingi mbinu ambazo tunatumia zinaathiri udongo ambapo baadaye inaharibu mazingira na kuathiri mazao. Ndio maana tupo hapa kuleta vichwa vyetu pamoja kama wadau kubuni mradi ambao utasaidia kukabili hali hiyo,” alisema Mudaki.


Kulingana na afisa katika shirika la the alternative youth, Caroline Atensen , mabadiliko ya tabia nchi ni moja ya maswala ambayo yanachangia pakubwa katika changamoto ya chakula duniani, na hivyo kunahitajika suluhu ya haraka kauli yake ikisisitizwa na Winnie Cheptoo kutoka shirika la SIKOM.


“Moja ya changamoto ambazo ulimwengu unakabiliwa nazo ni uhaba wa chakula ambao mara nyingi husababishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hivyo tunapata kwamba kilimo ni moja ya mbinu za kuhakikisha kwamba hilo linashughulikiwa,” alisema Bi. Atensen.


Kwa upande wake afisa wa kilimo kaunti ya Pokot magharibi Abraham Nang’ole alisema idara hiyo itashirikiana na shirika la Declares na wadau wengine katika kuhakikisha kwamba shughuli za kilimo zinaimarishwa kaunti hii.


“Tunafurahi kuwaarifu wakulima wetu kwamba tutakuwa tukishirikiana na Declares maeneo ya nyanjani kuhakikisha kwamba idara yetu ya kilimo inaimarishwa,” alisema Nang’ole.