Maonyesho ya kilimo Pokot Magharibi yafunguliwa rasmi

Na Emmanuel Oyasi,
Maonyesho ya kilimo katika kaunti ya Pokot magharibi yameanza rasmi wito, ukitolewa kwa wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza na kuhudhuria maonyesho hayo ambayo yanaandaliwa katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Kishaunet.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho hayo, naibu gavana Robert Komole alisema lengo kuu la kuandaliwa maonyesho hayo ni kutoa fursa kwa wakazi hasa wakulima kupata mafunzo kuhusu mbinu za kilimo ili kuimarisha uzalishaji na kukuza uchumi.
“Lengo kuu la maonyesho haya ya kilimo ni kuhakikisha sisi kama wakulima wa Pokot Magharibi tunapata fursa ya kuelemishwa kuhusu mbinu za kilimo ili kujimudu kimaisha,” alisema Komole.
Komole aliwataka wakazi kutochukulia maonyesho hayo kuwa mradi wa serikali ya kaunti bali fursa ya kipekee ya kupata maarifa kutoka kwa wataalam mbali mbali wa kilimo ambao watakuwa wakidhihirisha mbinu mbali mbali za kilimo.
“Nawarai wakazi wa kaunti hii kujitokeza kuhudhuria maonyesho haya, na kutoyachukulia kuwa mradi wa serikali, bali fursa ya kipekee ya kupata maarifa ya kilimo ili kuimarisha shughuli zao za kilimo,” alisema.
Kauli yake ilisisitizwa na waziri wakilimo na mifugo kaunti hiyo Wilfred Longronyang ambaye alisema maonyesho haya ni muhimu katika kukuza kilimo kaunti hi ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula na kukabili magonjwa kama vile utapia mlo.
“Maonyesho haya ya kilimo ni nafasi bora kwetu kupata jinsi ya kujitosheleza kwa chakula kupitia kilimo na kuepuka changamoto za kiafya kama vile utapia mlo, na pia kupata fedha kupitia shughuli za kilimo,” alisema Longronyang.
Baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo wameelezea matarajio makubwa kutokana na maonyesho hayo ikiwemo kuimarisha shughuli zao za kilimo kupitia mafunzo ambayo yanatolewa.