Hatutakubali kufadhaishwa na serikali ya Kenya kwanza; Kachapin

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameisuta vikali serikali kuu chini ya uongozi wa rais William Ruto kwa kile amedai inaendeleza juhudi za kuangamiza ugatuzi.
Akizungumza jumanne katika majengo ya bunge la kaunti hiyo, gavana Kachapin alisema serikali ya taifa imefanya mtindo hulka ya kuchelewesha fedha kwa serikali za kaunti hali ambayo inalemaza pakubwa shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Alisema kama baraza la magavana kamwe hawataruhusu serikali kuangamiza magatuzi kwani imekuwa nguzo ya maendeleo nchini.
“Serikali hii ya Kenya kwanza ni yangu niliipigania, lakini pahali palipo na kasoro lazima tuseme. Ugatuzi ni nguzo muhimu ya maendeleo nchini, na sisi kama magavana hatuwezi kuruhusu ugatuzi kuhujumiwa jinsi inavyofanya serikali kuu,” alisema Kachapin.
Aidha gavana Kachapin aliikosoa serikali kwa kuzilazimisha serikali za kaunti kutekeleza ununuzi na kutoa zabuni kupitia mfumo wa dijitali e-procurement, akisema kamwe magavana hawatakubali kushinikizwa kutumia mfumo ambao haujapitia mchakato unaohitajika kikatiba.
“Hatukatai kutumia e- procurement. Lakini haiwezekani ati sasa hazina ya kitaifa ndiyo itakuwa ndiyo inasema ni mtu fulani tumechagua kwa niaba Pokot magharibi kufanya kazi fulani. Hamjapata madhara ya hayo maneno,” alisema.
Kando na hayo gavana Kachapin alitetea utedakazi wake katika kipindi cha miaka mitatu ambayo amehudumu kama gavana wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi, akitaja sekta za afya na elimu kuwa zilizonawiri chini ya utawala wake.