Jukwaa la Husika lazinduliwa kukabili changamoto za mabadiliko ya hali ya anga

Na Emmanuel Oyasi,
Wadau katika sekta ya mazingira wamekongamana mjini Lodwar kaunti ya Turkana kuangazia mbinu ya kukabili changamoto za mabadiliko ya hali ya anga ili kuzuia athari ambazo hutokana na hali hiyo hasa katika kaunti za wafugaji.


Akizungumza na wanahabari afisa katika shirika la IGAD anayesimamia maeneo kame na ufugaji Roba Guyo alisema lengo kuu la kikao hicho ni kuweka mikakati ya kuwasaidia wakazi wa kaunti kame kupata habari mapema kuhusiana na hali ya anga ikiwemo kubuni jukwaa ambalo litawasaidia kubaini hali hizo.


“Tumekutana na wadau mbali mbali kujadili jinsi ambavyo tutaweza kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kikao hiki pia kimetumika kubuni jukwaa kwa jina husika ambalo litakuwa likitoa habari za mapema kuhusu maswala yoyote ambayo yanaweza kutokana na mabadiliko ya hali ya anga,” alisema Guyo.

Kulingana na afisa anayeshughulikia mfumo wa habari kijiografia GIS katika shirika hilo Andrew Maling’a, jukwaa hilo kwa jina Husika litasaidia wakulima na wakazi katika maeneo kame katika kubaini mapema hatari ambazo zinatokana na mabadiliko ya hali ya anga ikiwemo majanga kama vile mafuriko.


“Jukwaa hili limebuniwa kuangazia hatari ambazo zinaweza kutokana na mabadiliko ya hali ya anga, mfano, majanga kama vile mafuriko na hata ukame,” alisema Maling’a.


Kauli yake ilisisitizwa na naibu kamishina eneo la Pokot kaskazini kaunti ya Pokot magharibi mourice Ogwena ambaye aidha alisema jukwaa hilo linawaleta pamoja wadau kutoka sekta mbali mbali na kuwa na mkondo mmoja wa kutoa taarifa kwa jamii kuhusu hali mbali mbali.


“Jukwaa la Husika pia linatumika kuleta pamoja wadau kutoka sekta mbali mbali na kuwa kwenye mkondo mmoja ili wanapotoa taarifa kwa jamii kuhusu hali mbali mbali iwe ni moja,” alisema Ogwena.