Poghisio ashutumu mauaji ya watoto katika kaunti ya Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameshutumu vikali visa vya kupotea watoto na kupatikana wakiwa wameuawa, ambavyo vimeripotiwa kutekelezwa na raia kutoka taifa jirani la Uganda.
Katika mahojiano na kituo hiki, Poghisio alisema inasikitisha kwa matukio ya kinyama kama haya kuripotiwa katika kaunti hiyo hasa na raia wa taifa la kigeni.
Alipongeza juhudi za maafisa wa usalama kuwakamata washukiwa huku akiwataka kuhakikisha mhusika mkuu aliyetoweka anapatikana na kufikishwa mahakamani.
“Haya mambo ya kuua watoto nayalaani sana. Haiwezekani kwamba mambo kama haya yanafanyika katika kaunti yetu. Na kwa sababu baadhi yao wamekamatwa, nawaomba maafisa wa polisi kuhakikisha mhusika mkuu anapatikana na kuwajibishwa kisheria,” alisema Poghisio.
Aidha Poghisio aliunga mkono hatua ambayo ilichukuliwa na kamati ya usalama katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi ikiongozwa na kamishina wa kaunti Abdulahi Khalif kuagiza kupigwa msasa upya raia wote wa kigeni, akisisitiza haki kwa waathiri wa visa hivyo.
“Nakubaliana na agizo la kaunti kamishina kwamba wageni wote wakaguliwe upya, kwa sababu kaunti yetu ipo mipakani na huwezijua ni kina nani wanaingia,” alisema.
Alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kuwa watulivu wakati serikali inaposhughulikia swala hili huku akiwahimiza kuwa makini na watu ambao wanaishi karibu nao, ili kuzuia visa vya kinyama kama hivi kutokea siku za usoni.
“Nawaomba wakazi wawe na subira serikali inapoendelea kushughulikia swala hili. Lakini pia wanapasa kuwa makini na watu wanaoishi karibu nao na kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote ambaye wanamshuku,” aliongeza.