Raia kutoka mataifa ya kigeni wanaoishi Pokot Magharibi kukaguliwa upya

Na Benson Aswani,
Kamati ya usalama kaunti ya Pokot magharibi imeagiza raia kutoka mataifa ya kigeni ambao wanaishi katika kaunti hiyo kukaguliwa upya ili kuthibitisha uhalali wa vyeti vinavyowaruhusu kuendeleza shughuli zao katika kaunti hiyo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya kikao cha kamati hiyo, kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Abdulahi Khalif alisema hatua hii inajiri kufuatia visa vya kutoweka watoto na kupatikana wakiwa wameuawa, kuhusishwa na raia wa kigeni.
“Kamati ya usalama imeagiza kukaguliwa upya raia wote wa kigeni ambao wameshukiwa kuhusika na kupotea watoto kaunti hii ili kubaini uhalali wao na shughuli wanazofanya hapa,” alisema Khalif.
Khalif aliagiza kurejeshwa ardhi ya umma aliyekuwa akiishi mshukiwa mkuu wa visa hivyo ambaye anadaiwa kuwa raia wa taifa moja jirani, akisema majengo yote ambayo yapo kwenye ardhi hiyo yataondolewa mara moja.
“Mshukiwa mkuu ambaye amekiri kuua na kula mabaki ya watoto amekuwa akiishi katika ardhi ya serikali. Ardhi hiyo imetwaliwa na majengo yote yaliyo kwenye ardhi hiyo yatabomolewa mara moja,” alisema.
Aidha, Khalif alisema polisi wamezuia mipango ya baadhi ya vijana kuvamia kituo cha polisi cha Kapenguria kuwachukua washukiwa waliokuwa wakishikiliwa katika kituo hicho na kuwateketeza, pamoja na kukiteketeza kituo hicho, akiwaonya viongozi wa kisiasa aliosema wanawachochea wakazi kuchukua hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria.
“Kuna baadhi ya vijana ambao walikuwa wamepanga kuvamia kituo cha polisi cha Kapenguria kuwatwaa washukiwa ambao walikuwa wamezuiwa na polisi ili kuwachoma na kuteketeza kituo hicho, lakini tumeweza kuzuia mipango hiyo,” aliongeza.
Wakati uo huo Khalif alitumia fursa hiyo kutangaza kwamba watu 8 wameripotiwa kupotea kufikia sasa, wakiwemo watu wazima watatu na watoto watano, huku washukiwa 6 wakikiri kuwaua watoto sita ambao hawajaripotiwa.
Washukiwa waliokamatwa walifikishwa katika mahakama ya Kitale jumatatu ambapo mahakama iliupa upande wa mashitaka siku 21 kukamilisha uchunguzi kuhusiana na madai yanayowakabili kabla ya maelekezo zaidi kutolewa.