Msako wa raia wa kigeni wanaoishi Pokot magharibi bila Kibali waanzishwa

Na Emmanuel Oyasi,
Serikali imetangaza msako wa raia wa mataifa ya kigeni ambao wanaishi katika kaunti ya Pokot magharibi bila stakabadhi zinazowaruhusu kuwa hapa nchini.


Akizungumza kwa niaba ya kamishina, msaidizi wa kamishina kaunti hiyo Emily Ogolla alitoa agizo kwa maafisa wa polisi kwa ushirikiano na machifu kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba kuwatambua raia hao ili waweze kurejeshwa kwenye mataifa yao.


“Afisi inasema kwamba watu wote ambao wanaishi miongoni mwetu bila stakabadhi zinazofaa wanafaa kurudi katika nchi zao. Afisi imetoa agizo kwa maafisa wa polisi na machifu kufanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwatambua watu hawa na kuwarejesha kwao,” alisema Bi. Ogolla.


Aidha Bi. Ogolla alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kushirikiana na maafisa hao wa usalama katika kuwatambua raia hao kwa kuwasilisha majina yao na sehemu wanakoishi.


“Natoa wito kwa wakazi wa kaunti hii kushirikiana na maafisa hao kwa kutoa taarifa kuhusu watu ambao wanawafahamu kuishi kaunti hii bila stakabadhi hizo, ili kufanikisha shughuli hii,” alisema.


Kauli yake Ogolla ilifuatia lalama za wakazi wa kaunti hiyo pamoja na baadhi ya viongozi kuhusu ongezeko la raia wa mataifa ya kigeni kaunti hiyo bila stakabadhi hitajika, hali wanayodai kwamba imechangia ongezeko la utovu wa usalama.