Serikali ya Pokot Magharibi yawekeza pakubwa katika sekta ya afya

Na Benson Aswani,
Zaidi ya asilimia 30 ya bajeti ya serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeelekezwa kwenye idara ya afya kuhakikisha kwamba kuna dawa za kutosha katika hospitali na vituo vyote vya afya maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo.
Haya ni kwa mujibu wa gavana Simon Kachapin ambaye alisema serikali yake imejitolea kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa kaunti hiyo, ili kukabili changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika sekta hiyo.
Aidha Kachapin aliwataka wasimamizi wa zahanati na vituo vya afya kuhakikisha usimamizi bora wa vifaa vya matibabu ikiwemo dawa ambazo zinaelekezwa kwenye vituo hivyo, ili kuhakikisha wananchi hawapitii wakati mgumu wanapotafuta huduma za matibabu.
“Dawa hata kama ni ya milioni 30 ni nyingi iwapo itasimamiwa vizuri. Usimamizi bora ndicho kitu cha muhimu kwa kuwa vituo vya afya na dawa bila usimamizi ni kazi bure,” alisema gavana Kachapin.
Gavana Kachapin alisema serikali yake itaajiri wahudumu wapya zaidi 200 na kuwatuma kuhudumu katika vituo mbali mbali vya afya, ili kukabili upungufu wa wahudumu hao ambao umekuwa ukishuhudiwa katika vituo hivyo.
“Juma lijalo tunawatuma wahudumu wapya zaidi ya 242 katika vituo mbali mbali vya afya katika hatua ambayo itapunguza uhaba wa wahudumu katika vituo vyetu vya afya,” alisema.
Wakati uo huo Kachapin alisifia kuimarika sekta ya afya nchini hatua aliyosema imechangiwa na ujio wa serikali za magatuzi.
“Ugatuzi ulikuja ndipo tufanye uamuzi wetu kama kaunti hasa majukumu muhimu, ikiwemo jinsi ya kuimarisha idara ya afya. Na tumeona umesaidia sana kuimarisha hospitali zetu,” aliongeza.
Gavana Kachapin aliyasema hayo baada ya kupokea dawa za kima cha shilingi milioni 36 kutoka shirika la dawa la Meds ambazo zinatarajiwa kusambazwa katika vituo mbali mbali vya afya kaunti hii ya Pokot magharibi.