SERKALI KUU PAMOJA MASHIRIKA MBALIMBALI YAENDELEZA VITA DHIDI YA UKEKETAJI NA KUWAOZA MABINTI MAPEMA ENEO LA ALALE
Hafla ya maadhimisho ya kimataifa ya kukomesha ukeketaji ambayo imefanyika katika eneo la Alale kwenye kaunti ya Pokot Magharibi imewahusisha raia wa taifa la Uganda na wa taifa hili la Kenya.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mwandamizi katika wizara ya vijana na jinsia Rechael Shebesh amesema lengo la kuwaunganisha wakazi wa mataifa yote mawili ni kutokana na madai ya wasichana wengi nchini kutoroshwa na kuvushwa Uganda wakati wanapotaka kutekeleza ukeketaji pamoja ma wakati wa kuwaoza mabinti mapema. Vilevile wa Uganda hutorokea taifa hili ili kukwepa maafisa wa polisi wanaowasaka.
Shebesh ametumia fursa hiyo kuwaonya machifu dhidi ya kuzembea katika kazi zao huku vijiji kadhaa vikitajwa kuwa vingali vinaendeleza ukeketaji kwa wingi.
Vijiji hivyo ni pamoja na Kasitot, Simak, Nawyapong’, Akoret miongoni mwa vingine.
Mashirika mbalimbali yakishirikiana na serikali za kaunti na serikali kuu yameendeleza vita dhidi ya ukeketaji na kuwaoza mabinti mapema hasa miongoni mwa jamii za wafugaji nchini.
Kulingana na mke wa gavana wa kaunti ya Pokot Magharini John Lonyangapuo, Marry Lonyangapuo kwa upande wake ametaja vita hivyo kuwa vigumu iwapo serikali zote na washikadau wote katika jamii wasipoungana mikono katika kulikabili janga hilo.
Hata hivyo, Katibu mkuu katika wizara ya vijana na jinsia amesema zipo fedha serikalini za kufanikisha vita hivyo.