Mwili wa mtoto wapatikana umeoza shambani Bendera

Na Benson Aswani,
Idara ya upelelezi DCI imeanzisha uchunguzi baada ya mwili wa mtoto mwenye umri wa miaka saba kupatikana kwenye shamba la mahindi ukiwa umeanza kuoza katika eneo la Bendera kaunti ya Pokot Magharibi.
Ni hali ambayo ilipelekea bara bara ya Kitale Lodwar kufungwa kwa muda jumatatu usiku na kutatiza hali ya usafiri na nyumba za washukiwa kuteketezwa na wananchi wenye gadhabu katika eneo hilo.
Kulingana na Evans Nyachio, mzee wa mtaa huo, mwili huo ambao ulikuwa umeoza ulipatikana na vijana waliokuwa wakitafuta matunda.
Nyachio alisema kwamba licha ya hali yake mbaya, mwili wenyewe uliweza kutambuliwa na mamake marehemu na kuwa washukiwa wawili ambao ni raia wa taifa la Uganda walikuwa wamekamatwa wakishukiwa kuhusika na kupotea kwake.
“Kuna vijana walikuwa wakienda kwa shamba la jirani kula matunda ya mwitu. Walipoingia katika shamba la mahindi wakapata mwili ambao ulikuwa umeoza. Lakini mama ya mwenda zake aliweza kutambua kwamba ni mtoto wake. Kuna washukiwa ambao tayari wamekamatwa kwa kuhusishwa na kupotea mtoto huyo,” alisema Nyachio.
Nyachio aliongeza kwamba mtoto huyo alipotea tarehe 4 mwezi juni na juhudi za kumtafuta hazikufua dafu hadi wakati mwili wake ulipopatikana kwenye shamba la mahindi.
“Huyu mtoto alipotea tarehe 4 mwezi juni. Alitoka shuleni, akakula chakula na kutoka na wenzake kwenda kucheza. Kutoka wakati huo mtoto hakurudi hadi vyenye amepatikana akiwa amefariki,” alisema.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika chumba cha wafu cha hospitali ya rufaa ya kapenguria huku uchunguzi ukianzishwa kuhusiana na kisa hicho.