Viongozi wa Kenya kwanza kaskazini mwa bonde la ufa watetea utawala wa rais Ruto

Na Benson Aswani,
Wandani wa rais William Ruto kutoka kaskazini mwa bonde la ufa wamepuuzilia mbali miito ambayo inatolewa ya kumtaka rais Ruto kuondoka mamlakani kwa madai ya kushindwa kuliendesha taifa, wakishikilia kwamba rais Ruto atamaliza mihula yake miwili ilivyo kikatiba.


Akizungumza katika hafla ya harambee kwenye kanisa la IBET eneo la Sigor kaunti ya Pokot magharibi, gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Jonathan Bii aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo pamoja na viongozi kwa ujumla kushirikiana na kuunga mkono utawala wa rais Ruto kwa ajili ya maendeleo.

“Mheshimiwa Mwai Kibaki aliongoza kwa mihula miwili, Uhuru kenyatta akaongoza kwa mihula miwili, na sasa Ruto pia ni lazima ataenda kwa mihula miwili. Sisi wote tukae pamoja tuunge mkono rais wetu ili tufanikishe maendeleo,” alisema Bii.


Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin alishutumu maandamano ambayo yaliandaliwa juma lililopita dhidi ya utawala wa rais William Ruto akiyataja kuwa mabaya zaidi kuliko hata ugaidi kutokana na uharibifu ambao ulishuhudiwa.


Alivitaka vitengo vya usalama kufanya uchunguzi kwa upesi ili kuwakamata waliochochea maandamano hayo ambayo alisema yaliingiliwa na wahalifu, na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa kuhujumu amani ya taifa.


“Bila amani nchi yetu haiwezi kuendelea. Na ndio maana sisi kama viongozi hatuungi mkono maandamano ya uharibifu. Tumeona maandamano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini ni ya uharibifu mkubwa hata kuliko vitendo vya kigaidi,” alisema Kachapin.