Komole awashutumu viongozi kwa kuendeleza siasa za mapema Pokot Magharibi

Na Benson Aswani,
Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ameshutumu siasa za mapema ambazo zinaendelezwa na viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katika mahojiano na kituo hiki Komole alisema inasikitisha kuona viongozi wakiwa tayari wamebuni mirengo ya kisiasa kwa nia ya kuendeleza azma zao za kuwania nyadhifa za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, wakati wakazi wanatarajia maendeleo kutoka kwao.
Komole alisema siasa ambazo zinaendelezwa na viongozi hao zimehujumu juhudi za kuwahakikishia wakazi maendeleo, kwani wengi wa viongozi wanatumia muda wao mwingi kusukuma ajenda zao, akiwahimiza kukoma hulka hiyo na kuzingatia huduma kwa wananchi.
“Siasa zimeanza kuchacha mapema katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Matarajio yetu kama serikali ya kaunti ilikuwa kwamba kutakuwa na ushirikiano miongoni mwa viongozi kuwahakikishia wananchi maendeleo, lakini viongozi wamesahau hayo na kujitosa katika siasa za uchaguzi,” alisema Komole.
Aidha Komole alisema ni siasa hizi ambazo zimepelekea kaunti hiyo kutonufaika na nyadhifa katika serikali kuu kutokana na viongozi kutoshikana mikono kusukuma ajenda za kaunti kwa serikali kuu jinsi inavyoshuhudiwa katika kaunti jirani.
“Hatujaweza kunufaika kutoka kwa serikali kuu jinsi tulivyotarajia kwa sababu ya migawanyiko ambayo ipo miongoni mwa viongozi. Tukiangalia majirani zetu wana maafisa wengi katika serikali kuu ila sisi hatuna uwakilishi ambao tunaweza kujivunia kwamba tupo serikalini,” alisema.