SERKALI YA KITAIFA YAPIGA JEKI UJENZI WA SHULE ZA MIPAKANI

POKOT MAGHARIBI


Serikali ya kitaifa ikishirikiana na serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi imeendelea kupiga jeki ujenzi wa shule za maeneo ya mipakani ikiwa ni njia mojawapo ya kudumisha amani baina ya jamii za Turkana, Pokot, na Marakwet.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabweni na madarasa katika Shule ya Msingi ya Moi iliyoko katika eneo la Masol ambayo yamejengwa na serikali kuu kupitia Idara ya Kukabili Changamoto za Ukame Nchini NDMA, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amewapongeza viongozi ambao wamefanikisha ujenzi wa shule hizo zilizoko katika maeneo ya mipakani.
Wamalwa ameahidi kuwa wizara yake itafanikisha miradi mbalimbali katika kaunti ya Turkana na Kaunti ya Pokot Magharini ukiwamo mradi wa unyunyuziaji mashamba ikiwa ni njia mojawapo ya kuinua uchumi kukomesha vita dhidi ya jamii hizo mbili.
Wakati uo huo amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali katika Kaunti ya Pokot Magharibi wakishirikiana na wazazi kuwapeleka wanao shuleni kwa faida zao za baadaye.