Serikali ya Pokot Magharibi yawahakikishia wakazi uzinduzi wa basari mwezi Julai

Na Benson Aswani,
Baada ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kusubiri kwa muda fedha za basari kutoka kwa serikali ya kaunti, naibu gavana Robert Komole hatimaye amewahakikishia wakazi kwamba serikali ya gavana Simon Kachapin itatoa fedha hizo mapema mwezi julai mwaka huu.


Katika mahojiano na kituo hiki, Komole alisema gavana Kachapin amekuwa akishughulikia baadhi ya maswala ambayo yalipelekea fedha hizo kuzuiliwa ikiwemo kutia saini makubaliano na wizara ya kitaifa ya elimu pamoja na kutuma rasmi maombi kwa afisi ya mdhibiti wa bajeti.


Japo alikiri hali ya kuzuiliwa fedha hizo ilichangiwa pia na siasa za baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi, Komole alisema juhudi za gavana Kachapin kuandaa vikao vya mazungumzo vya mara kwa mara na mdhibiti wa bajeti vimepelekea fedha hizo kuachiliwa rasmi.


“Kuna siasa ambazo ziliingizwa kwenye maswala ya basari hadi fedha hizo zikasimamishwa, lakini gavana wetu aliweza kung’ang’ana, akitia saini na wizara ya elimu pamoja na kuzungumza na mdhibiti wa bajeti, na sasa tunaweza kusema kwa ujasiri kwamba basari itapeanwa tarehe 4 mwezi julai kule Chesta,” alisema Komole.


Komole aliwashukuru wakazi wa kaunti hiyo kwa kuwa na subira wakati ambapo serikali ya kaunti chini ya gavana Kachapin imekuwa mbioni kuhakikisha kwamba vikwazo ambavyo vimekuwa vikizuia fedha hizo kutolewa kwa kaunti vinashughulikiwa.


“Nawashukuru sana watu wetu kwa kuwa na subira kipindi hiki chote. Haikuwa mapenzi ya serikali ya gavana kuchelewesha basari, bali ilikuwa tu mswala ya siasa na pia kisheria. Lakini sasa vikwazo vimeondolewa na basari itapeanwa,” alisema.


Ikumbukwe serikali ya gavana Kachapin kwa muda sasa imekuwa ikimlaumu seneta wa kaunti hiyo kwa madai ya kuchochea kuzuiliwa basari, kufuatia maswali aliyoibua katika kikao cha kamati ya seneti kuhusu matumizi ya fedha kwenye serikali za kaunti.