Kikundi cha Her Lab, Murpus chapongezwa kwa kuwaimarisha kina mama kiuchumi

Na Benso Aswani,
Wajasiriamali kutoka mashirika mbali mbali nchini walikutana jumatano na makundi ya kina mama eneo la Murpus katika kaunti ya Pokot magharibi kubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kujiwezesha na kuimarisha shughuli zao kiuchumi.


Mhasisi wa vivo Fashion Group mmoja wa wajasiriamali hao kutoka jijini Nairobi Wandia Gichuru alisema wanatumia fursa hiyo pia kutoa mafunzo kwa kina mama hao kuhusu jinsi ya kujiwezesha kifedha huku akielezea kuridhishwa na hatua ambazo wamepiga kufikia sasa.


“Tumekuwa na mazungumzo na kina mama kuhusu jinsi ya kujiimarisha kiuchumi na jinsi ambavyo wanapanga kuimarisha jamii zao. Na tunafurahia kile ambacho tumeona na kusikia kwani wamebadilisha sana maisha yao,” alisema Bi. Gichuru.


Flora mutahi mhasisi wa shirika la Melvins tea alipongeza kikundi cha Her Lab ambacho kimekuwa kikihusika pakubwa katika kuwaokoa wanaopitia dhuluma za kijinsia na kuwapa mafunzo ya jinsi ya kujiimarisha kiuchumi, wengi wao wakiwa tayari wanaendeleza miradi mbali mbali.


“Kile ambacho napenda sana kuhusu hiki kikundi cha Her Lab ni kwamba kinawapa kina mama hawa maarifa ya jinsi ambavyo wataweza kujiimarisha kiuchumi, na tupo hapa kuwaunga mkono katika shuguli zao,” alisema Bi. Mutahi.


Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la Perur Rays of Hope Carolyne Menach alielezea matumaini ya mpango huo kuleta mageuzi katika jamii, kando na kubadili hali ya kiuchumi ya wanaonufaika na mpango huo.


“Ni mpango ambao unahakikisha kwamba kuna mageuzi katika jamii kutokana na maarifa ambayo wanapata hapa na ambayo yatawasaidia kuimarisha familia zao kiuchumi na jamii kwa jumla,” alisema Bi. Menach.


Kina mama ambao wamehusika mpango huo walielezea jinsi ambavyo wamenufaika kiuchumi na kubadili maisha yao pakubwa.