Poghisio alalamikia madhara yanayosababishwa na kiwanda cha saruji cha Sebit

Na Emmanuel Oyasi,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameelezea haja ya kupanuliwa kiwanda cha saruji cha Sebit ili kiwe na uwezo wa kutengeneza simiti kikamilifu na kuzuia hali ya saruji kutoka katika kiwanda hicho kusafirishwa hadi maeneo mengine.


Poghisio alisema hatua hii itasaidia kuimarisha usalama wa barabara hasa ya kutoka Chepareria kuelekea ortum, kwani itapunguza msongamano wa malori ya kubeba Saruji ambayo kulingana naye yamekuwa yakisababisha ajali nyingi kwenye barabara hiyo.


Aidha Poghisio alisema kando na kuwa nyembamba mno kwa magari hayo, barabara hiyo pia imeharibiwa na uzito ambao hubebwa na magari hayo yanaposafirisha saruji kueleka maeneo mengine nje ya kaunti ya Pokot magharibi.


“Tuliambiwa kiwanda cha kutengeneza simiti kitajengwa huku kuzuia kusafirishwa saruji hadi maeneo mengine, kwa sababu ilivyo kwa sasa barabara zetu hazipo salama. Malori yanayobeba saruji yanamaliza barabara na ni mazito, hali hii inaharibu sana barabara zetu,” alisema Poghisio.


Poghisio aliwalaumu viongozi wa kaunti hiyo kwa kuwa wepesi wa kuzungumzia maswala yao ya kisiasa na kulifumbia macho swala hili, ambalo alisema kwamba ni muhimu zaidi kwa ajili ya usalama wa wakazi wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi.


“Ni kwa sababu gani viongozi wetu wamenyamaza kuhusu swala hili? Wanatumia muda wao mwingi kupiga siasa na kusahau maswala muhimu ambayo yanawahusu watu wetu,” alisema.