Shughuli ya uchimbaji dhahabu yasitishwa rasmi Pokot magharibi

Na Emmanuel Oyasi,
Serikali ya kitaifa imeagiza kufungwa mara moja zaidi ya migodi 500 ambayo imekuwa ikitumika kuchimba dhahabu katika kaunti ya Pokot magharibi.
Akizungumza Jumatatu baada ya kikao na wadau katoka sekta mbali mbali, kamishina wa kaunti hiyo Abdulahi Khalif alisema hamna shughuli zozote za uchimbaji dhahabu ambazo zitaruhusiwa kwenye machimbo hayo.
Tangazo hilo linajiri baada ya mtu mmoja kuaga dunia baada ya kufukiwa na mchanga wakati akiendeleza shughuli hiyo eneo la kambi karaya Jumapili jioni.
Kulingana na Khalif, katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita watu saba wameaga dunia kwenye migodi wakiendeleza shughuli hiyo ya kuchimba dhahabu.
“Serikali imetoa agizo la kufungwa migodi yote ya dhahabu kaunti hii ya Pokot magharibi. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, watu saba wameaga dunia katika machimbo ya dhahabu, na hatuwezi kuendelea hivi,” alisema Khalif.
Wakati uo huo Khalif alisema kwamba shughuli hiyo ya uchimbaji haramu wa dhahabu inasababisha uharibifu wa mazingira, mto Turkwel ukiathirika kwani maji yake sasa si salama kwa matumizi.
“Shughuli hii ya uchimbaji madini isiyodhibitiwa imepelekea uharibifu mkubwa wa mazingira. Tunavyozunvumza sasa Mto Tukwel si salama kwa matumizi kutkana na harakati hizi za kuchimba dhahabu,” alisema.