Wizara ya madini yaweka mikakati ya kudhibiti uchimbaji madini Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Wizara ya madini imezindua afisi yake mjini Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi katika juhudi za kuimarisha sekta hiyo na kuhakikisha kwamba shughuli ya uchimbaji madini inatekeleza kwa mujibu wa sheria.
Ni hatua inayojiri huku swala la uchimbaji madini usiofuata taratibu ambazo zipo kisheria likiendelea kuibua hisia mseto miongoni mwa viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi, ambao wametaka serikali kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba raslimali za kaunti hiyo zinalindwa.
Katibu wa utawala katika wizara ya madini David Onyancha alisema lengo la kufunguliwa afisi hiyo ni kuhakikisha kwamba shughuli ya uchimbaji madini katika kaunti hii inadhibitiwa.
“Ningependa kusisitiza kwamba serikali ipo makini katika kuhakikisha shughuli ya uchimbaji madini inadhibitiwa, na kufunguliwa afisi hii kutasaidia kuhakikisha hilo linaafikiwa hasa katika kaunti hii ambapo uchimbaji madini unatajwa kuendeshwa kiholela,” alisema Onyancha.
Mkurugenzi wa kitengo cha kutoa leseni katika wizara hiyo Gregory Kituku alisema kwamba ufunguzi wa afisi hiyo utasaidia kuleta huduma karibu na mwananchi na kusaidia pakubwa kudhibiti ajali ambazo zinatokea kwenye migodi kutokana na uchimbaji madini usiyo wa kisheria.
“Tumekuja hapa kufungua afisi hii ili kuleta huduma karibu na wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi, na kuhakikisha kwamba shughuli ya uchimbaji madini inafanyika kulingana na sheria ili kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kutokana na shughuli ya uchimbaji madini isiyodhibitiwa,” alisema Kituku.
Kwa upande wake naibu kamishina wa Kapenguria Wyclife Munanda alisema kwamba shughuli katika idara ya madini kaunti hiyo hazitakuwa kama kawaida kwani sasa kutakuwa na mwanzo mpya baada ya kuzinduliwa rasmi afisi hiyo.
“Hali haitakuwa kama kawaida. Sasa kutakuwa na mwanzo mpya kuhusiana na shughuli hii nzima ya uchimbaji madini,” alisema Munanda.