KVDA yasambaza miche kwa shule za bonde la Kerio

Mkurugenzi mkuu wa KVDA Sammy Naporos akishiriki zoezi la upanzi wa miche, Picha/Angela Cherono

Na Emmanuel Oyasi,
Mamlaka ya mandeleo eneo la Kerio Valley KVDA inapeana miche milioni moja na laki sita katika shule kwenye kaunti za bonde la kerio katika juhudi za kuafikia malengo ya serikali ya upanzi wa miche bilioni 15.


Akizungumza alhamisi katika shule ya upili ya Chepkorniswo eneo la chepareria katika kaunti ya Pokot magharibi, mkurugenzi mkuu wa KVDA Sammy Naporos alisema miongoni mwa miche hiyo, laki sita ni miche ya matunda ili kuafikia ajenda ya utoshelevu wa chakula nchini.

“Tunapeana miche milioni moja na laki sita katika shule za eneo hili katika juhudi za kuafikia lengo la rais William Ruto la kupanda miche bilioni 15. Kati ya hiyo laki sita ni miche ya matunda,” alisema Naporos.


Kwa upande wake mkurugenzi wa maendeleo ya kanda kwenye wizara ya maswala ya afrika mashariki Wanjiku Manyata alisema ni jukumu la kila mmoja kushiriki shughuli ya upanzi wa miche kuafikia malengo.


“Ni jukumu letu sisi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli ya upanzi wa miche. Na si kupanda tu bali tuhakikishe pia kwamba miche tunayopanda tunaitunza vyema,” alisema Manyata.


Aidha mamlaka hiyo ilizindua shughuli ya kuchimba kisima eneo la Chepkat, mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Chepkat Martin Jumwa akipongeza hatua hiyo aliyosema itawafaa zaidi ikizingatiwa eneo hilo limekuwa na tatizo la maji kwa muda.


“Sehemu hii imekuwa na tatizo la maji kwa miaka mingi sana. Wakazi huku wamekuwa wakilazimika kwenda mwendo mrefu kutafuta maji lakini sasa tunafurahia mradi huu ambao utakuwa suluhu kwa tatizo hili,” alisema jumwa.