Wakfu wa Safaricom waikabidhi zahanati ya Kreswo vifaa vya matibabu

Maafisa kutoka wakfu wa safaricom wakikabidhi zahanati ya Kreswo vifaa vya matibabu,Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Zahanati ya Kreswo katika wadi ya Riwo kaunti ya Pokot magharibi imepigwa jeki baada ya kupokezwa vifaa vya matibabu kutoka wakfu wa Safaricom kupitia mkakati wake wa Pamoja Scheme Initiative, ambavyo vinanuiwa kuimarisha huduma katika zahanati hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhi uongozi wa zahanati hiyo vifaa hivyo, meneja mkuu wa uhasibu katika kampuni ya Safaricom Judy Mwangi, alisema vifaa hivyo vitasaidia sana hasa katika kuhakikisha afya ya kina mama ambao wanafika katika zahanati hiyo kujifungua.
“Tunashukuru sana kwa sababu tunaona kina mama sasa wameboreshewa huduma za afya na wanaweza sasa kujifungua kwa urahisi na kupata tiba kamilifu bila ya kupitia mahangaiko,” alisema Bi. Mwangi.
Ni hatua ambayo ilipongezwa pakubwa na wahudumu katika zahanati hiyo wakiongozwa na Emily Partany ambao walisema vifaa hivyo vitasaidia pakubwa katika kusuluhisha changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo katika kuwahudumia wanaotafuta huduma.
“Tunafurahia sana hawa watu wa Safaricom ambao wamekuja kuturahisishia shughuli zetu za kuwapa huduma za afya wakazi wa eneo hili hasa kina mama. Tumekuwa tukipitia changamoto sana kwa muda katika kutoa huduma za afya,” alisema Partany.
Hata hivyo wahudumu hao walilalamikia kupitia changamoto kuwasajili wakazi wa eneo hilo katika bima ya afya ya jamii SHA kutokana na idadi kubwa ya wakazi kukosa vitambulisho vya kitaifa, na changamnoto ya mtandao.
“Changamoto ambayo tupo nayo sasa ni kuwasajili wakazi katika bima ya afya ya jamii SHA. Kina mama wengi ambao wanakuja kujifungua hawana vitambulisho vya kitaifa sasa inafanya vigumu kuwasajili kwenye bima hiyo,” alisema.