Viongozi Pokot magharibi wazidi kuteta kuhusu uchimbaji haramu wa madini

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong akiwa na baadhi ya wanaochimba madini, Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia kile wamedai uchimbaji madini kinyume cha sheria katika ardhi ya kaunti hiyo.


Akizungumza jumanne eneo lake la uwakilishi, mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alisema wachimbaji madini ambao wanatumia mashine mbali mbali kuendeleza shughuli hiyo bila ya stakabadhi za kuwaruhusu kujishughulisha na uchumbaji madini, wameharibu pakubwa mazingira maeneo husika.


Hata hivyo, Lochakapong alisema wakazi wa kaunti hiyo ambao kwa kawaida hujihusisha na shughuli hiyo kwa viwango vidogo kwa ajili tu ya kujikimu kimaisha wanafaa kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao.


“Nimesema mara nyingi kwamba kuna watu ambao wanachimba madini kaunti hii kinyume cha sheria. Hatuna tatizo na watu wetu ambao wanachimba madini kwa kiwango kidogo kwa ajili tu ya matumizi yao ya kila siku, lakini wale wanaotumia mashine kutekeleza shughuli hii wanafaa kufuata sheria,” alisema Lochakapong.


Wakati uo huo Lochakapong alidai kwamba licha ya Mahakama kutoa agizo la kusitisha shughuli hiyo, wapo baadhi ya watu ambao wanatumia njia za mkato kutaka kurejelea uchumbaji haramu wa madini, hali aliyosema huenda ikasababisha mizozo miongoni mwa wakazi.


“Jambo la kushangaza ni kwamba licha ya kuwa shughuli hii ilisitishwa rasmi na mahakama, kuna watu ambao wanajaribu kutumia njia za mkato kutaka kurejelea shughuli hiyo,” alisema.