Wabunge wasimama tisti na NG-CDF

Samwel Moroto Mbunge wa Kapenguria, Picha/Maktaba
Na Emmanuel Oyasi,
Wabunge nchini wameendelea kutetea hazina ya ustawishaji maeneo bunge NG-CDF wakitofautiana na pendekezo la kinara wa chama cha ODM Raila Odinga la kutaka hazina hiyo kuondolewa mikononi mwa wabunge, na badala yake fedha hizo kuongezwa kwa mgao unaotolewa kwa magavana.
Kulingana na mbunge wa Kapenguria, kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto, wengi wa wanafunzi wataathirika zaidi iwapo hazina hiyo itaondolewa, akitaka kiwango cha fedha hizo kuongezwa ili kuwanufaisha wananchi zaidi badala ya kuondolewa.
Moroto alisema vikao vya kuwahusisha wananchi kutoa maoni kuhusu hatima ya hazina hiyo vitasaidia kuifanya kutambuliwa rasmi kikatiba, na kuziba mianya inayotumiwa na wale aliowataja kuwa wasio na nia njema kwa hazina hiyo ya NG-CDF.
“Mambo ya CDF, mtu asijaribu kusema kwamba kuna kitu atatoa. Tunashukuru serikali kwa sababu imetupa nafasi ya kuwahusisha wananchi katika swala hili, na tunaenda sasa kuipitisha bungeni, iwe sheria ili wale wajuaji wasianze kuturudisha nyuma,” alisema Moroto
Kauli yake Moroto ilisisitizwa na wadau katika sekta ya elimu wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya ELCK Annet eneo bunge la Sigor Joel Atutikichan, ambaye alisema wengi wa wanafunzi eneo hilo wanasalia shuleni kutokana na basari ambazo zinatolewa katika hazina hiyo.
Alisema wazazi wengi eneo hilo wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha na hivyo kuwa vigumu kwao kupata fedha za kuwalipia wanao karo, wakisalia kutegemea basari zinazotolewa na wabunge.
“Tangu tufungue shule wanafunzi wengi wamesalia nyumbani kwa sababu hawana karo. Lakini waliposikia basari inazinduliwa, tulishuhudia wanafunzi wengi wakianza kuja shule. Hii ina maana kwamba basari inategemewa sana na watu wetu,” alisema Atutikichan.