NG-CDF yaungwa mkono pakubwa shughuli ya kukusanya maoni ikiingia siku ya pili

Wakaazi wa sigor wakishiriki vikao vya maoni kuhusu NG-CDF, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Shughuli ya kutoa maoni kuhusu hazina ya ustawishaji maeneo bunge NG-CDF inaingia jumanne siku ya pili huku wabunge wakiwa mbioni kuhakikisha wanafanyia marekebisho kipengee cha katiba ili kutambuliwa rasmi hazina hiyo iliyotangazwa na mahakama kuwa kinyume cha sheria.


Katika siku ya kwanza ya vikao hivyo jumatatu, wananchi maeneo mbali mbali ya kaunti ya Pokot magharibi walipinga vikali pendekezo la kuondolewa hazina hiyo chini ya usimamizi wa wabunge.


Wakizungumza katika vikao vya kuchukua maoni kuhusu mswada huo, wakazi eneo la Sigor wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Masol Wilson Chekeruk, walisema hazina ya NG-CDF imekuwa ya manufaa makubwa hasa katika sekta ya elimu ambapo imewawezesha wengi wa wanafunzi kupokea elimu kupitia basari.


“Wadi ya Masol ni moja ya wadi ambazo zimetengwa katika maswala ya maendeleo. Lakini tunavyozungumza sasa CDF imeboresha pakubwa eneo hilo kimaendeleo. CDF pia imekuwa yenye manufaa makubwa hasa katika sekta ya elimu ambapo wengi wa wanafunzi kutoka jamii masikini wamepata fursa ya kuendelea na masomo yao,” alisema.


Akizungumza kwa niaba ya idara ya usalama, msaidizi wa kamishina eneo hilo Peter Njuguna alisema kwamba idara ya usalama pia imenufaika chini ya hazina hiyo kupitia ujenzi wa miundo mbinu ili kuimarisha doria za maafisa wa usalama pamoja na kujenga vituo vya polisi.


“CDF imetusaidia sana katika shughuli zetu. Kupitia hazina hii miundo msingi imeboreshwa hasa barabara ambapo sasa maafisa wetu wanaendeleza doria bila changamoto za barabara mbovu ilivyokuwa awali. Pia afisi zetu zimejengwa kupitia hazina hiyo,” alisema Njuguna.


Kwa upande wao viongozi kaunti hiyo wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong walipuuzilia mbali kauli ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba NG-CDF iondolewe chini ya usimamizi wa wabunge, wakimtaka kusubiri maoni ya wakenya kabla ya kutoa msimamo wake.


“Aliyekuwa waziri mkuu ametoa msimamo wake kuhusu CDF. Lakini msimamo wake usiwe ndio anataka utekelezwe. Lazima asubiri maoni ya wakenya kuhusu hazina hii kabla ya kutoa msimamo wake,” alisema Lochakapong.


Shughuli hiyo ya kutoa maoni kuhusu hazina ya NG-CDF ilianza jumatatu na inatazamiwa kuendelea hadi alhamisi Mei 8.