Hofu huku visa vya uvamizi vikianza kuchipuka tena Kerio Valley

David Chepelion afisa mkuu wa maswala ya amani kaunti ya pokot magharibi, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Wadau mbali mbali wa usalama katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuelezea wasiwasi kuhusu kuchipuka upya visa vya utovu wa usalama, ambavyo vimeshuhudiwa katika siku za hivi karibuni mipakani pa kaunti za bonde la Kerio.


Katika kikao na wanahabari afisini mwake, afisa mkuu wa maswala ya amani kaunti hiyo David Chepelion alisema mikutano ya amani ambayo iliandaliwa na viongozi mbali mbali wa kaunti hizi na juhudi za maafisa wa usalama, zilipelekea kushuhudiwa hali ya utulivu ila sasa visa vya utovu wa usalama vimeanza kuripotiwa tena.


“Tulikuwa tumefanya mikutano kadhaa ya kuleta watu pamoja, na hatua hiyo ilikuwa imepelekea kushuhudiwa usalama maeneo haya lakini sasa tunaona visa vya uhalifu vimeanza tena kurejea,” alisema Bw. Chepelion.


Chepelion alisema kwamba visa hivi vinatekelezwa na wahalifu ambao wanaendelea kumiliki bunduki haramu, akielezea haja ya kuendeshwa oparesheni ya kuondoa bunduki zinazomilikiwa kinyume cha sheria na wakazi maeneo hayo.


“Kuna watu ambao bado wanamiliki bunduki haramu katika eneo hili la bonde la Kerio, hali ambayo imepelekea kuongezeka visa hivi. Serikali inapasa kuendesha oparesheni ya kuondoa silaha hizi mikononi mwa raia,” alisema.


Wakati uo huo kiongozi huyo alitoa wito kwa waziri wa usalama Kipchumba Murkomen kushirikiana na viongozi wa kaunti za bonde la kerio na wadau katika sekta ya usalama eneo hilo katika kuhakikisha kwamba visa hivi vinakabiliwa.


“Naomba sana waziri wa usalama ashirikiane kikamilifu na viongozi kutoka kaunti hizi wanaoendeleza juhudi za kuhakikisha amani inarejea kikamilifu eneo hili,” aliongeza.