Poghisio aitaka serikali kukoma mtindo wa ukopaji

Samwel Pogihisio aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi, Picha/Maktaba
Na Benson Aswani
Miito imeendelea kutolewa kwa uongozi wa serikali ya kenya kwanza chini ya rais William Ruto kupunguza madeni ambayo inakopa kutoka mataifa ya nje.
Wa hivi punde kutoa wito huo ni aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye ameelezea hofu kwamba huenda taifa likafikia kiwango ambacho litashindwa kulipia madeni hayo iwapo mkondo wa sasa wa ukopaji utaendelea.
“Deni la taifa limezidi sana hata mapato yetu. Rais anapasa kujaribu kupunguza mkondo wa ukopaji wa madeni ili tusipitishe kiwango ambacho tutashindwa kulipa,” alisema Bw. Poghisio.
Poghisio ambaye aliwahi kuhudumu kama kiongozi wa wengi katika bunge la seneti alisema ni wakati taifa hili linapasa kujisimamia kwa kuhakikisha raslimali zilizopo nchini zinatumika vyema, ili kuzuia hulka ya ukopaji ambayo huenda ikaliweka taifa pabaya.
“Ningeomba tuangalie sana hili jambo. Ni vyema sisi tujisimamie badala ya kwenda kuomba omba zaidi kuliko jinsi mapato yetu yanaweza kulipa,” alisema.
Wakati uo huo seneta huyo wa zamani alilitaka bunge la kitaifa kubuni sheria za kuzuia ufisadi ambao umekuwa chanzo cha matumizi mabaya ya fedha za mlipa ushuru, ili fedha ambazo zinapotea kupitia ufisadi zitumike katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
“Bunge letu lianze kutengeneza sheria ambazo zitasaidia kupunguza visa vya ufisadi ili pesa ambazo zinapotea kupitia ufisadi zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo,” aliongeza.