Mwanamme amkatakata mwenzake wakizozania mwanamke

Na Benson Aswani,
Polisi makutano kaunti ya Pokot magharibi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa ambapo mwanamme mmoja mwenye umri wa makamu anadaiwa kukatwakatwa kwa upanga hadi kufa kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mzozo wa kimapenzi.


Ni kisa ambacho kilitokea usiku wa kuamkia jumatano kwenye chumba kimoja cha burudani mjini Makutano alikokuwa anavinjari.


Kulingana na mhudumu wa chumba hicho cha burudani, mwanamme huyo ambaye alitambuliwa kwa jina Peter na ambaye ni fundi wa kuunganisha mambomba ya maji, alikatwa kichwani mara mbili kwa upanga na mwanamme ambaye alidai kupokonywa mkewe.


“Ilikuwa mwendo wa saa mbili usiku ambapo huyu mwanamke ambaye anazozaniwa alipiga mayowe akiitisha pikipiki, tulipofika eneo la tukio kufahamu ni nini tukamkuta Peter akiwa chini anavuja damu nyingi baada ya kukatwa kwa upanga,” alisema mhudumu.


Mmoja wa mashuhuda wa kisa hicho Stephen Githinji alisema mwathiriwa alikuwa anaishi na mwanammke husika kama mkewe kwa muda mrefu baada yake kutengana na aliyekuwa mmewe kwa kipindi cha miaka mitatu kabla yake kurejea na kutekeleza unyama huo.


“Huyu mwanamke aliachana na mmewe miaka mitatu iliyopita na akaamua kuolewa na mwanamme mwingine. Sasa huyu mwanamme ambaye alikuwa naye wa kwanza amekuja na machungu na kutekeleza unyama huu,” alisema Githinji.


Githinji alitoa wito kwa wanandoa kufuata sheria wakati wanapotalikiana ili kuzuia visa kama hivi kutokea
“Wito wangu kwa wanandoa ni kwamba kama kweli mmeamua kutengana, tafadhali fanya hivyo kisheria ili kila mtu afahamu kwamba hana uhusiano tena na mwenzake ili kuzuia visa kama hivi,” alisema.