Ajali ya ndege iliyomwangamiza Ogolla ilipangwa; Kalonzo

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akiwahutubia wanahabari, Picha/Maktaba
Na Emmanuel Oyasi,
Viongozi wa mrengo wa upinzani wameendelea kutilia shaka ripoti ya uchunguzi wa kiini cha ajali ya ndege iliyomwangamiza mkuu wa majeshi jenerali Francis Ogolla pamoja na wanajeshi wengine tisa wa KDF.
Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema ripoti hiyo iliyopokezwa rais William Ruto ijumaa wiki iliyopita sio ya kuaminika kwani uchunguzi haukuendelezwa na mamlaka huru.
Akiongea na wanahabari, kalonzo alisema kwamba ripoti hiyo ya uchunguzi ina mianya na ilitolewa tu ili kuwapumbaza wakenya.
“Ripoti hii imetolewa ili kuwafumba macho wakenya kuhusu kilichotokea katika jail hiyo. Hakuna mtu ambaye ataamini kilicho kwenye ripoti hiyo. Njia ya pekee ya kuamini ripoti kuhusu uchunguzi wa ajali hii ni kuwa na kitengo huru kuendesha uchunguzi,” alisema Bw. Kalonzo.
Bw. Kalonzo alidai kwamba ajali iliyomuua Ogolla ilipangwa na watu fulani.
“Ogolla alitumwa na baraza la kitaifa la usalama katika jumba la Bomas kabla ya matokeo ya uchaguzi kutolewa, na baadhi ya watu walisema kwamba watakabiliana naye vilivyo,” alidai.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi, ajali hiyo ilisababishwa na matatizo kwenye injini ya ndege iliyokuwa imembeba Ogolla na wenzake.
Katika ripoti hiyo, wizara ya ulinzi ilisema kwamba ndege hiyo aina ya Huey Helicopter KAF 1501 ilikaguliwa vyema na ikathibitishwa kuwa katika hali nzuri, na kwamba ilikuwa imetumika katika oparesheni kadhaa ikiwabeba watu mashuhuri.
“Ndege hiyo ilikuwa ikiendeshwa na watu wenye uzoefu mkubwa. Ila kulingana na manusura, baada ya kukumbwa na matatizo ya injini, marubani walijaribu kuidhibiti ili itue salama ila wakashindwa,” ilisema ripoti.
Ogolla aliaga dunia tarehe 18 mwezi aprili mwaka 2024 katika ajali iliyotokea eneo la sindar kaunti ya Elgeiyo Marakwet.
Inaarifiwa ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 12 wakiwemo maafisa wa ngazi ya jenerali kabla ya kuhusika ajali.
Ni mtu mmoja pekee anayeaminika kuwa mpiga picha aliyenusurika ajali hiyo.