4 wajeruhiwa na Chui Riwo, wakazi wakiishi kwa hofu

Mmoja wa waathiriwa wa uvamizi wa chui, Picha/Maktaba

Na Benson Aswani,
Wakazi wa kijiji cha Kalapochoni kata ndogo ya Poole wadi ya Riwo kaunti ya Pokot magharibi wanaishi kwa hofu kufuatia kukithiri visa vya uvamizi wa wanyamapori.


Hii ni baada ya watu wanne waliokuwa wakivuna mchanga kuvamiwa na chui aliyetokea kichaka kimoja sehemu waliyokuwa, kabla ya kusaidiwa na wakazi ambao waliwakimbiza katika hospitali ya Kacheliba level 4.


Kisa hicho cha jumatatu kimewatia hofu wakazi eneo hilo wakiongozwa na John Lokor ambao wametoa wito kwa huduma ya wanyamapori KWS kumsaka chui huyo kabla ya kusababisha madhara zaidi.


“Tunaishi kwa hofu huku kwa sababu tangu kisa hicho chui huyo hajakamatwa na hatujui mahali yuko. Tunaomba huduma ya KWS kuharakisha na kumshika mnyama huyo na kumrudisha mahali anastahili kukaa kabla asababishe madhara zaidi,” alisema Lokor.


Hata hivyo siku moja tu baada ya nne hao kujeruhiwa na chui, mkazi mmoja eneo lilo hilo anakadiria hasara baada mbuzi wake kuuliwa na chatu.


Chifu wa kata ya Riwo Philip Lepkou alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuwa waangalifu na kutoa taarifa kuhusu mnyama yeyote anayeweza kuleta madhara, akiwatahadharisha pia dhidi ya kukaribia maeneo ya misitu.


“Nawahimiza wakazi kuwa waangalifu na kutokaribia misitu kiholela ili kuzuia uvamizi wa wanyama. Na iwapo kuna taarifa yoyote kuhusu kuonekana mnyama anayeweza kusababisha hatari, wawasilishe katika idara husika,” alisema Lepkou.


Akizungumzia kisa hicho kupitia taarifa, naibu kamishina kaunti hiyo Wyclife Munanda alisikitikia kisa hicho akitoa wito kwa huduma ya wanyamapori KWS kuchukua hatua za haraka kumtafuta chui huyo na kumnasa kabla ya kusababisha madhara zaidi.