Haitakuwa njia rahisi kwa Ruto kurejea ikulu; Poghisio

Rais Wiliam Ruto katika moja ya ziara zake za maendeleo, Picha/Maktaba
Na Emmanuel Oyasi,
Rais William Ruto atalazimika kukabiliwa na wakati mgumu katika safari yake ya kuwania awamu ya pili ya urais wa taifa kwenye kinyang’iro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katika mahojiano na kituo hiki, aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio, alisema kwamba huu ni wakati ambapo rais Ruto anapasa kuanza kufikiria kuhusu watu ambao atashirikiana nao katika safari yake kuelekea ikulu kwa muhula wa pili.
Alisema wengi wa wandani wa rais wamekuwa wakimhadaa kwamba hali inaendelea vyema nchini chini ya utawala wake, wakati hata rais mwenyewe anafahamu fika kwamba mambo hayaendi sawa.
“Rais Ruto atakabiliana na pambano tofauti na lile alilokabiliana nalo mwaka 2022. Huu ni wakati ambapo anafaa kuzingatia kwa makini watu wanaompa ushauri kuhusu hali ilivyo nchini. Si wale wanaomhadaa kwamba hali ni shwari wakati mwenyewe anafahamu hali si nzuri,” alisema Poghisio.
Wakati uo huo, Bw. Poghisio alitumia fursa hiyo kumshauri rais kukoma kutoa ahadi zaidi kwa wakenya, wakati ahadi ambazo alitoa wakati wa kampeni hazijashughulikiwa kikamilifu.
Alisema rais ana muda wa kujikomboa kutoka katika hasira ya wakenya, iwapo atatumia vyema muda wake uliosalia kabla ya kukamilika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wake kama rais wa taifa hili.
“Rais anapasa kukoma kutoa ahadi juu ya zingine. Anafaa kutekeleza yake aliyoahidi kwanza. Na iwapo atatumia vyema muda wake uliosalia vyema huenda akajikomboa kutoka hasira ya wakenya,” alisema.