Serikali ipo mbioni kudhibiti hasara inayosababishwa na radi

David Chepelion afisa mkuu katika idara ya majanga kaunti ya Pokot magharibi, Picha/Benson Aswan

Na Benson Aswani,
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi chini ya gavana Simon Kachapin inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba visa vya radi maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo vinakabiliwa.


Katika kikao na wanahabari afisini mwake, afisa mkuu katika idara ya majanga kaunti ya Pokot magharibi David Chepelion alisema kumeshuhudiwa visa vya radi maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo ambapo wakazi wamekadiria hasara kutokana na hali hiyo.

“Mojawapo ya mikakati ambayo kaunti imeweka ni sheria ya kuzuia radi. Awali gavana wetu aliweka vifaa vya kudhibiti radi ila kwa sasa tuna mikakati maalum ambayo tunataka kuhakikisha vifaa hivyo vinawekwa sehemu ambazo zina changamoto hiyo,” alisema Chepelion.


Chepelion alisema idara hiyo imefanya uchunguzi katika sehemu mbalimbali za kaunti hiyo na kubaini maeneo ambayo yanakabiliwa na hatari kubwa ya kushuhudia visa hivyo, akielezea hatua ambazo serikali ya kaunti inachukua kuvikabili.


“Tumezuru maeneo mbalimbali ya kaunti hii na kubaini sehemu ambazo zinahitaji sana kuwekwa vifaa vya kudhibiti radi. Tuna wahisani ambao tumejaribu kuzungumza nao na watakuja kutusaidia,” alisema.


Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi wa maeneo hayo kuwa makini na kuzingatia kanuni za usalama ili kuzuia kupigwa na radi, ikiwemo kutotembea miguu tupu nyakati za mvua na kutojikinga mvua chini ya miti.


“Nawaambia watu wetu kwamba wajilinde. Wasitembee miguu tupu hasa nyakati za mvua wala kujikinga mvua chini ya miti ili kuzuia kupigwa na radi,” aliongeza.