Mulongo aahidi kupanda miti kwa juhudi baada ya kupokonywa sindano

Debora Barasa Mulongo Akipanda miti,Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Waziri wa afya anayeondoka Debora Barasa Mulongo amepongeza hatua ya rais William Ruto kumteua kuwa waziri wa mazingira katika mabadiliko ya hivi punde ambayo yametekelezwa na rais katika baraza lake la mawaziri.
Akizungumza alhamisi wakati akiongoza zoezi la upanzi wa miti eneo la Lomukee wadi ya Lelan eneo bunge la Pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi, Mulongo aliahidi kujitolea katika wizara hiyo mpya kuhakikisha kwamba lengo la serikali kupanda miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032 linaafikiwa.
“Namshukuru sana rais kwa kunipa nafasi hii kusimamia hii wizara. Naahidi kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuhakikisha kwamba lengo la serikali kupanda miche bilioni 15 kufikia mwaka 2032 linatimia,” alisema waziri Mulongo
Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi kukumbatia zoezi la upanzi wa miti akisema kwamba mbali na kukabili mabadiliko ya tabia nchi, miti ni muhimu katika kuhakikisha utoshelevu wa chakula, dawa na kuimarisha rutuba ya mchanga miongoni mwa manufaa mengine.
“Kwa hivyo nawasihi wakazi wa kaunti hii kukumbatia zoezi hili la upanzi wa miti kwani miti ina faida nyingi sana ikiwemo kuhifadhi mchanga, chakula na hata dawa,” alisema.
Kauli yake ilisisitizwa na afisa mkuu katika idara ya maji, mazingira mali asili na tabia nchi Leonard Kamsait ambaye alisisitiza ushirikiano wa serikali ya kaunti na serikali kuu kuhakikisha hilo linaafikiwa.
“Kama serikali ya kaunti ya Pokot magharibi tunashirikiana kikamilifu na serikali kuu kuhakikisha kwamba lengo la miche bilioni 15 linaafikiwa ili tulete suluhu kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Kamsait.
Mulongo alihamishwa kutoka wizara ya afya hadi wizara ya mazingira iliyokuwa ikisimamiwa na Aden Duale ambaye alihamishiwa wizara ya afya katika mabadiliko ya hivi punde yaliyofanywa na rais William Ruto katika baraza lake la mawaziri.