Viongozi Pokot Magharibi walaumiwa kwa wakazi kutopata teuzi katika serikali kuu

Daktari Samwel Poghisio,Picha / Maktaba
Na Benson Aswani,
Aliyekuwa seneta wa kaunti ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amewasuta viongozi katika kaunti hiyo kwa kile alisema kutochukua hatua yoyote kuwatetea wakazi kupata nafasi katika serikali ya kitaifa.
Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Poghisio alisema licha ya rais William Ruto kufanya teuzi mbali mbali katika serikali yake, kaunti hiyo haijanufaika popote hali aliyosema imechangiwa na viongozi wa sasa kutopendekeza majina ya wakazi wa kaunti hiyo katika nyadhifa hizo.
“Tatizo katika kaunti hii ni kwamba wale ambao wako uongozini hawashughuliki kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti hii wanapata nyadhifa katika serikali kuu,” alisema Poghisio.
Aidha Poghisio alitaja migawanyiko ambayo inashuhudiwa miongoni mwa viongozi katika kaunti hiyo kwa kubuni mirengo ya kisiasa kuwa swala ambalo linafanya vigumu kwa wakazi kuteuliwa serikalini.
“Changamoto hapa ni kwamba viongozi wetu wamegawanyika katika mirengo, na labda wanaona kwamba wakimpendekeza mtu fulani huenda akawa kutoka mrengo ambao hawaungi mkono, sasa hii inafanya vigumu kwao kuwatetea kaunti hii kitaifa,” alisema.
Seneta huyo wa zamani sasa anatoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi kuwa makini zaidi katika uchaguzi mkuu ujao, na kuwachagua viongozi ambao watawajibika katika kuhakikisha kwamba kaunti hiyo pia inazingitiwa wakati wa kubuni serikali ijayo.
“Mimi naomba kwamba siku moja wakazi wa kaunti hii watambue kwamba viongozi kama hawa hawawezi kuwasaidia, hivyo wasiwarudishe tena uongozini kwa sababu ni wabinafsi, hawataki watu wengine wapate kazi,” aliongeza.