Ubalozi wa Ireland wazuru pokot magharibi kukagua miradi ya maendeleo

Neale Richmond- Balozi wa Ireland Nchini Kenya,Picha/Benson Aswan
Na Emmanuel Oyasi,
Ujumbe kutoka ubalozi wa Ireland nchini Kenya umezuru jumatano kaunti ya Pokot magharibi na kukagua miradi mbali mbali ambayo inaendelezwa chini ya ufadhili wa taifa hilo.
Balozi wa taifa hilo hapa nchini Neale Richmond aliyeongoza ujumbe huo, alisema serikali ya Ireland itaendelea kushirikiana na serikali ya kaunti hiyo kupitia miradi mbali ambayo inanuiwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Tumekuwa na ushirikiano mzuri na kaunti hii ya Pokot magharibi na tunaahidi kuhakikisha kwamba ushirikiano huu unaendelea ili tukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa pamoja,” alisema Bw. Richmond.
Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema kupitia ushirikiano huo kaunti ya Pokot magharibi imeweza kukabiliana na changamoto ya uhaba wa raslimali hasa kwa jamii ya wafugaji na ambayo imekuwa chanzo cha utovu wa usalama hasa maeneo ya mipakani.
“Uhaba wa maji na lishe kwa mifugo ndicho chanzo kikuu cha mizozo ambayo imekuwa ikishuhudiwa miongoni mwa jamii za wafugaji kutokana na kung’ang’ania raslimali chache zilizopo. Ushirikiano huu umesaidia kupunguza mizozo hii kufuatia miradi ambayo inaendelezwa,” alisema Kachapin.
Aidha Kachapin alipongeza kiwango ambacho serikali ya Ireland imewekeza katika kaunti hiyo hasa miongoni mwa vijana anaosema kwamba wamepewa fursa kubwa ya kuwa wabunifu na kujistawisha katika ulimwengu huu wa teknolojia.
“Tunashukuru sana kwa maisha ambayo taifa hili limegusa kupitia kuwekeza katika kaunti hii. Wengi wa vijana wamenufaika kupitia uwekezaji huo hasa kupitia ubunifu katika ulimwengu huu wa teknolojia,” alisema.