Kaunti ya Pokot magharibi imepiga hatua kukabili dhuluma za kijinsia

Bi. Scovia kachapin, Mkewe Gavana Wa Kaunti Ya Pokot Magharibi, Picha / Benson Aswan.
Na Emmanuel Oyasi,
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali ya kijamii imejitolea kuhakikisha kwamba tamaduni iliyopitwa na wakati ya ukeketaji inakabiliwa.
Haya ni kwa mujibu wa mkewe gavana wa kaunti hiyo Bi. Scovia Kachapin ambaye alisema serikali inaendelea kuweka mikakati itakayohakikisha tamaduni hii pamoja na ndoa za mapema zinakabiliwa, ili kuwapa watoto wa kike fursa ya kutimiza ndoto zao kupitia elimu.
Bi. Scovia ambaye alikuwa akizungumza katika hafla moja eneo la Murpus, alisema afisi yake inaendeleza mradi wa kuwasaidia kina mama ambao walilazimika kusitisha masomo yao kutokana na sababu mbali mbali kujiendeleza kimaisha, kwa kuwanunulia vifaa vitakavyowasaidia kujitafutia riziki.
“Ukeketaji umekuwa kizungumkuti katika kaunti hii ya Pokot magharibi. Serikali yetu kwa ushirikiano na washirika mbali mbali wamekuwa wakisaidiana kuhakikisha kwamba visa hivi vinakabiliwa,” alisema Bi Scovia.
Akizungumza katika hafla hiyo, waziri wa jinsia, michezo na vijana Bi. Lucky Litole alisema afisi yake imebuni sheria ambazo zitasaidia katika kukabili visa vinavyohusu dhuluma za kijinsia, na kuhakikisha wanawake pia wanahisi salama na kuheshimika katika jamii.
“Tuna sheria ambazo tumebuni, sheria kuhusu jinsia, kuwalinda watoto pamoja na sheria kuhusu vijana ambazo zinatusaidia kufanya kazi vyema kwa ushirikiano na washirika wetu kuhakikisha kwamba tunapunguza visa vya dhuluma za kijinsia,” alisema Bi. Litole.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la Perur Rays of Hope Bi. Carolyne Menach alisema kupitia shirika hilo wamefanikiwa kuwawezesha kina mama zaidi ya 750 kupitia miradi ambayo inawanufaisha kiuchumi.
“Kama shirika tumeweza kuwasaidia zaidi ya kina mama 750 kwa kuwapa mtaji wa kuanzishia shughuli zao za kibiashara ili kujimudu kimaisha. Kwa hivyo tunashukuru kuchangia katika kuwawezesha kina mama,” alisema Bi. Menach.
Siku ya kimataifa ya wanawake iliadhimishwa tarehe 8 Machi 2025 miito ya kuwawezesha wanawake katika jamii ikitawala hafla zilizoandaliwa maeneo mbali mbali ya nchi.