SERIKALI KUU IMECHELEWA KUNUNUA MAZAO YA WAKULIMA KWENYE KAUNTI YA TRANS NZOIA
Wakulima wa mahindi katika kaunti ya Trans Nzoia wamelalamikia hatua ya serkali kuchelewesha shughuli ya kununua mazao yao kwenye maghala ya bodi ya mazao na nafaka NCPB licha ya kutangazwa kwa bei mpya ya shilingi alfu mbili na mia tano kwa kila gunia la kilo tisini.
Mwenyekiti wa shirikisho la wakulima nchini tawi la Trans Nzoia Wiliam Kimoson anasema wakulima wengi wanapitia hali ngumu wakati huu ambapo wanatarajia kunufaika na kilimo hicho.
Kimoson hata hivyo amelalamika kwamba wengi wa wakulima hao wako kwenye mikopo na hasa kuhusu karo ya shule miongoni mwa mahitaji mengine.
Kadhalika Kimoson amesema wengi wa wakulima sasa wanalazimika kuwauzia wafanyibiashara matapeli kwa bei ya chini huku akisema kuwa bei ya mahindi inafaa kuwa angalau shilingi alfu tatu ili mkulima aweze kunufaika ikilinganishwa na gharama ya juu ya uzalishaji.