IDADI KUBWA YA WANAFUNZI WALIOJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA YAPELEKEA UHABA WA MIUNDO MSINGI KATIKA SHULE MBALI MBALI

Na Benson Aswani.

Uongozi wa shule ya upili ya wasichana ya St. Bakhita Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi umetoa wito kwa wahisani kujitokeza na kutoa ufadhili ambao utahakikisha kwamba shule hiyo inakuwa na miundo msingi bora.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Grace Kakuko alisema shule hiyo ilipokea wanafunzi wengi katika zoezi la usajili wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka huu hali ambayo imepelekea uhaba wa madarasa pamoja na mabweni.

Tuliwapokea wanafunzi wengi sana mwaka huu hadi sasa hatuna madarasa ya kutosha na mabweni ya kukidhi idadi hii kubwa ya wanafunzi. Tunaomba wahisani na viongozi kujitokeza ili kutusaidia katika kujenga madarasa na bweni jipya.” Alisema Bi. Kakuko.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Bw. Samwel Urieng alisema licha ya kwamba shule hiyo iliongeza bweni moja idadi ya wanafunzi waliosajiliwa mwaka huu imepelekea kutumika sehemu panaposimamishwa basi la shule kama sehemu ya kulala baadhi ya wanafunzi.

“Tulijaribu mwaka jana tukajenga bweni moja tukidhani kwamba litatosha, lakini mwaka huu wanafunzi wa kidato cha kwanza wamekuja wengi hadi tumeamua tena kutumia sehemu ambako basi husimamishwa kama sehemu ya kulala baadhi ya wanafunzi.” Alisema Bw. Urieng.

Wito huu ulikaririwa na wanachama wa bodi ya shule hiyo ambao walisema uhamasisho wa wadau mbali mbali kwa wakazi kuhusu umuhimu wa elimu kwa wanao ulipelekea ongezeko la idadi ya wanafunzi ambao walijiunga na shule hiyo.

Mwaka huu tumekuwa na wanafunzi 265 wa kidato cha kwanza ambao wamejiunga na shule hii. hii ni kutokana na uhamasisho ambao umekuwa ukiendelezwa na wadau kwa jamii kuhusu umuhimu wa wanao kupata elimu. Hivyo tunashukuru mashirika mbali mbali ambayo yalishiriki katika juhudi hizi.” Walisema.