MABWENI MATATU YA SHULE YA UPILI YA KIWAWA YATEKETEA.

Shule ya upili ya wavulana ya Kiwawa eneo la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi https://kalyafm.co.ke/mabweni-matatu-ya-shule-ya-upili-ya-kiwawa-yateketea/

Na Emmanuel Oyasi.

Shule ya upili ya wavulana ya Kiwawa eneo la Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi inakadiria hasara baada mabweni matatu ya shule hiyo kuteketea usiku wa kuamkia jumatatu katika kile kinachokisiwa kuwa hitilafu kwenye mfumo wa kusambaza umeme.

Akithibitisha kisa hicho mwalimu mkuu wa shule hiyo Luke Lutukoi hata hivyo alisema hamna mwanafunzi ambaye alijeruhiwa katika mkasa huo kwani ulitokea mwendo wa saa kumi unusu alfajiri wakati wanafunzi wakiwa katika masomo ya ziada.

Alisema kwamba bidhaa zote za wanafunzi zilizokuwa katika mabweni hayo ziliteketea katika mkasa huo japo hali ilidhibitiwa kwani walimu wote walikuwa shuleni wakati ukizuka.

“Hii leo mwendo wa saa kumi unusu alfajiri wakati wanafunzi wakiwa darasani kwa masomo ya asubuhi, mabweni matatu yalishika moto na kuteketea. Hamna chochote ambacho kiliokolewa katika mabweni hayo. Hata hivyo hali iliweza kudhibitiwa kwani walimu wote walikuwa shuleni wakati huo.” Alisema Lutukoi.

Alikana uwezekano wowote wa kisa hicho kusababishwa na wanafunzi akisema kwamba uchunguzi wa awali umethibitisha kwamba moto huo ulisababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa kusambaza umeme.

“Uchunguzi wetu wa awali umebaini kwamba moto huo ulisababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa kusambaza umeme. Kwa hivyo mtu asiseme kwamba ulisababishwa na wanafunzi. Wanafunzi wote wapo shuleni na wana utulivu.” Alisema.

Lutukoi alisema kwamba wanafunzi waliopoteza bidhaa zao kwenye mkasa huo wataendelea kupokea ushauri ili kuwatuliza.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wahisani kujitokeza na kuwasaidia wanafunzi hao ili waweze kuendelea na masomo yao bila ya kutatizika.