MIRADI YA KILIMO YAPUNGUZA DHULUMA ZA KIJINSIA POKOT MAGHARIBI.
Na Benson Aswani.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la centre for indigenous child right katika kaunti ya Pokot magharibi Evelyn Prech amepongeza miradi ambayo ilianzishwa na shirika hilo kwa ushirikiano na mashirika mengine katika kuhakikisha kwamba visa vya dhuluma za kijinsia vinapungua kaunti hiyo.
Prech alisema kwamba shirika hilo liliweza kuangazia maswala makuu ambayo yanapelekea kukithiri visa hivyo ikiwemo, umasikini, mabadiliko ya hali ya anga pamoja na utovu wa usalama.
Aidha amesema wengi wa kina mama maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo ambako miradi hiyo inatekelezwa, sasa wanajihusisha na maswala ya kilimo na ufugaji na kujitenga na tamaduni kama vile ukeketaji, pamoja na kutowategemea zaidi waume zao hali ambayo imepunguza visa vya dhuluma za kijinsia.
“Tulijaribu kabisa kusuluhisha swala la dhuluma za jinsia. Kwa ushirikianop na washirika wengine tulichimba visima ambapo kwa sasa wengi wa akina mama wanajihusisha na kilimo na hawategemei zaidi waume zao hali ambayo imepunguza pakubwa visa vya dhuluma za jinsia.” Alisema Prech.
Wakati uo huo Prech aliwahimiza wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuzingatia umuhimu wa kuwapeleka watoto wa kike shuleni ili pia waweze kutimiza malengo yao na kubadili maisha yao na ya jamii kwa ujumla.
“Tukimsomesha mtoto wa kike, kwa njia moja au nyingine atabadilisha mazingira yetu. Kwa hivyo nawahimiza wazazi kuhakikisha kwamba mtoto wa kike pia anapata elimu kama wenzao wa kiume.” Alisema.