BABA AKAMATWA KWA KUWADHULUMU WANAWE KINGONO LOMUT.

Na Benson Aswani.

Visa vya dhuluma dhidi ya watoto vimeendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo ya kaunti ya Pokot magharibi licha ya juhudi za serikali na baadhi ya mashirika ya kijamii kuhakikisha kwamba visa hivyo vinakabiliwa.

Hii ni baada ya jamaa mmoja kutoka eneo la Lomut eneo bunge la Sigor kaunti ya Pokot magharibi kukamatwa na maafisa wa polisi kwa madai ya kuwadhulumu kingono wanawe wawili wa kike.

Kulingana na mwanaharakati wa haki za watoto kaunti hiyo Irene cheruto ambaye amekuwa akifuatilia swala hilo, si mara ya kwanza kwa jamaa huyo kuendeleza dhuluma dhidi ya jamii yake kwani amewahi kukamatwa kwa kumjeruhi mkewe kwa panga, ila akaachiliwa baada ya kuomba msahama kwa mahakama na pia kusamehewa na jamaa zake.

Cheruto alisema kwamba visa vya dhuluma dhidi ya watoto vimeripotiwa kuongezeka kaunti hiyo nyingi ya visa hivyo vikihusu watu wa jamii za waathiriwa.

“Visa vya dhuluma dhidi ya watoto vimeenea sana katika baadhi ya maeneo ya kaunti hii ya Pokot magharibi, nyingi ya visa hivyo vikitekelezwa na jamaa za waathirika. Mfano kisa cha Lomut ambapo baba aliwadhulumu watoto wake wawili.” Alisema Cheruto.

Alitoa wito kwa mashirika mbali mbali ya kijamii kushirikiana ili kuhakikisha kwamba visa hivi vinakabiliwa na kuwapa watoto mazingira bora kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Alisema watoto hao wanaendelea kupewa mawaidha kwani wametatizika pakubwa kimawazo ikizingatiwa uovu huo ulitekelezwa na mtu ambaye walimwona kuwa kinga yao.

“Watoto hawa wanaendelea kupokea ushauri kwa sababu ni kisa ambacho kimewaathiri zaidi kisaikolojia ikizingatiwa wametendewa unyama huu na mtu ambaye walimzingatia kuwa kinga yao. Naomba mashirika zaidi kujitokeza na kushirikiana ili kukabili visa hivi.” Alisema.