WAZAZI WATAKIWA KUWAPELEKA MAPEMA WANAO WANAOJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA SHULENI ILI KUSAJILIWA.
Na Benson Aswani.
Shughuli ya kuwasajili wanafunzi wanaojiunga na shule za upili ikiendelea, wito umetolewa kwa wazazi wa wanafunzi ambao bado hawajaripoti katika shule walizoitwa kuhakikisha watoto wao wanaripoti katika shule hizo mapema iwezekanavyo.
Akizungumza wakati wa kuwasajili wanafunzi ambao wanajiunga na shule hiyo, naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Chewoyet kaunti ya Pokot magharibi Amos Gisike, alisema kwamba ni vyema kwa zoezi hilo kuharakishwa ili shughuli za masomo zianze mara moja.
“Tunatarajia wanafunzi 480 kujiunga na shule hii katika kidato cha kwanza na kufikia sasa tumeridhishwa na idadi ambayo imefika japo tunatarajia zaidi. Nawahimiza wazazi ambao bado hawajawaleta watoto wao, kufanya hivyo kwa haraka kwani tunatarajia kukamilisha zoezi haraka na kuanza masomo mara moja.” Alisema Gisike.
Hata hivyo Gisike alisema kwamba baadhi ya wanafunzi ambao wanajiunga na shule hiyo wana changamoto ya karo wengi wao wakiwa waliokuwa wakitegemea ufadhili kutoka kwa hazina ya maendeleo ya maeneo bunge CDF ila fedha hizo hazijatolewa hadi kufikia sasa.
“Kuna baadhi ya wanafunzi ambao wanatoka katika jamii zisizojiweza kifedha na walitarajia ufadhili kutoka kwa hazina ya maendeleo kwa maeneo bunge CDF ila bado hawajapata. Hiyo ndiyo changamoto ya pekee ambayo tumeshuhudia ila zoezi la kuwasajili linaendelea vyema.” Alisema.
Wazazi ambao wamewaleta watoto wao kusajiliwa kwenye shule hiyo walielezea kuridhishwa na jinsi shughuli hiyo inavyoendeshwa japo wakilalamikia kugharamika zaidi katika kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata mahitaji kabla ya kusajiliwa katika shule wanazojiunga nazo.
“Nashukuru usimamizi wa shule hii kwa sababu wamepangilia vyema zoezi hili. Tunachukua muda mfupi sana kwa watoto wetu kusajiliwa. Changamoto tuliyo nayo ni kwamba uchumi wa sasa umetufanya kugharamika zaidi kununua vifaa hitajika.” Walisema.