WIZARA YA ELIMU YATAKIWA KUHAKIKISHA CHAKULA CHA KUTOSHA KWA SHULE ZA MIPAKANI POKOT MAGHARIBI.
Na Emmanuel Oyasi.
Mbunge wa Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong amemtaka waziri wa elimu Ezekiel Machogu kubuni sheria ambayo itahakikisha kwamba chakula hakikosekani katika shule za maeneo ya mipakani.
Akizungumza katika hafla moja wadi ya Lomut, Lochakapong alisema ni sharti kuwe na mikakati ya kutosha kuhakikisha kwamba wanafunzi katika shule zilizoathirika na utovu wa usalama maeneo hayo ya mipakani wanahudhuria masomo bila ya changamoto yoyote.
Aidha alitaka wizara ya mipango maalum kuweka mikakati ya kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo wanapata msaada wa chakula kila baada ya miezi mitatu.
“Waziri wa elimu anapasa kubuni sheria ambayo itahakikisha kwamba shule za maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama mipakani zinapata chakula kila wakati. Pia wizara ya mipango maalum ihakikishe kwamba wakazi wa maeneo haya wanapata chakula baada ya kila miezi mitatu.” Alisema Lochakapong.
Wakati uo huo Lochakapong alitoa wito kwa tume ya huduma za walimu TSC kuwaajiri wakazi waliohitimu kutoka maeneo ambayo yanaathirika na utovu wa usalama kufunza katika shule za maeneo hayo, ili kuzuia hali ambapo walimu wanalazimika kuyakimbia maeneo hayo kutokana na mazingira magumu ya kufanyia kazi.
“Tume ya huduma kwa walimu TSC inafaa kuwaajiri wakazi wa maeneo haya ambao walihitimu katika taaluma ya ualimu ili wafunze katika shule za maeneo haya. Hii itazuia hali ambapo walimu wanalazimika kuhama kutokana na mazingira magumu ya kufanyia kazi.” Alisema.