KACHAPIN: NI WAKATI WA KUHAKIKISHA AHADI TULIZOTOA KWA WANANCHI WAKATI WA KAMPENI ZINATEKELEZWA.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kutilia mkazo umuhimu wa maafisa wote wa serikali kutekeleza majukumu ambayo walikabidhiwa ili kuhakikisha kwamba wananchi wanafurahia matunda ya uamuzi waliofanya katika uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza katika hafla moja mjini Makutano, gavana Kachapin alisema kwamba serikali ya Kenya kwanza chini ya rais William Ruto iliahidi kutekeleza maswala mengi kuhakikisha kwamba maisha ya wananchi yanaboreshwa na sasa ni wakati ambapo ahadi hizo zinapasa kutekelezwa.
Kachapin alisema nia yake pamoja na ya rais kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yanashuhudia utovu wa usalama hasa mipakani pa kaunti ya pokot magharibi yanapata amani na shughuli za kawaida kurejelewa, ikiwemo kufunguliwa shule zilizofungwa ni lazima itekelezwe, na ni jukumu la maafisa waliokabidhiwa wajibu huo kuhakikisha kwamba hilo linatimizwa.
“Tuliahidi kuwatekelezea wananchi mambo mengi ikiwemo kuhakikisha kwamba hali ya usalama inarejelewa mipakani pa kaunti hii na kuruhusu shughuli za masomo kuendelea. Sasa ni wakati ambapo tunafaa kutekeleza hilo, na ni jukumu la wanaohusika kuhakikisha kwamaba hilo linatimizwa.” Alisema Kachapin.
Kauli yake ilisisitizwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye aidha amesisitiza umuhimu wa kushughulikiwa kwa haraka utata unaokumba ardhi ya Chepchoina ambao alisema kwamba huenda ukapelekea tatizo kubwa la kiusalama baina ya wakazi wa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Trans nzoia.
“Haya mambo ya Pokot na Turkana yataisha. Lakini tatizo kuu ni hili la chepchoina ambalo linatishia kuleta uhasama kati ya jamii za pokot na zile za kaunti ya Trans nzoia. Hili ni tatizo ambalo linafaa kushughulikiwa kwa dharura kabla ya hali kuwa mbaya zaidi.” Alisema Moroto.