SWALA LA USALAMA BONDE LA KERIO LATAWALA FAINALI ZA KOMBE LA MURKOMEN POKOT MAGHARIBI.
Waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen amedokeza kuhusu mipango ya kuwafadhili wanafunzi 10 wanaojiunga na kidato cha kwanza katika kila jamii ambazo zinapakana kwenye bonde la kerio ambao watakuwa mabalozi wa amani kama njia moja ya kuhakikisha amani inadumishwa meneo haya.
Akizungumza katika fainali za kombe la Murkomen ambazo zilichezwa katika uwanja wa makutano kaunti ya Pokot magharibi, Murkomen alisema kwamba ufadhili huo utakuwa unatolewa kila mwaka, huku pia akielezea mpango wa kujengwa barabara za kiusalama katika kaunti hizi.
“Tunawafadhili wanafunzi kumi kutoka kila jamii katika kaunti za Kerio valley ambao wanajiunga na kidato cha kwanza ili wabadilishe eneo hili. Katika mipangilio yangu pia, kuna barabara za kiusalama ambazo tunatarajia kujenga maeneo haya ili kuimarisha usalama.” Alisema murkomen.
Waziri wa michezo Ababu Namwamba ambaye alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu serikalini ambao walihudhuria fainali hizo alisema kwamba idara yake inatoa nafasi sawa za kudhihirisha vipawa miongoni mwa vijana kaunti za bonde la kerio zikipewa kipau mbele.
“Ukipatia pembe zote za nchi nafasi, talanta zitaonekana. na sisi tutapatia pembe zote za Kenya nafasi za kudhihirisha talanta. Hii ndio maana tumefungua vituo 42 vya talanta kaunti za bonde la kerio zikipewa kipau mbele.” Alisema Namwamba.
Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin alitoa wito kwa waziri wa michezo Ababu Namwamba kuimarisha hali ya uwanja wa michezo wa Makutano kama njia moja ya kuhakikisha vijana wanaimarisha vipawa vyao.
“Kwanza namshukuru waziri Ababu kwa kuja hapa. Ombi langu tu ni kwamba akaweze kutusaidia kuimarisha uwanja huu wa michezo, ili tuwape vijana wetu mazingira bora ya kuimarisha talanta zao hasa katika sekta ya michezo.” Alisema Kachapin.
Baadhi ya viongozi ambao walihudhuria hafla hii akiwemo katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala walisisitiza haja ya wakazi wa kaunti zote za bonde la kerio kuzingatia umuhimu wa kuishi kwa amani ili kuruhusu serikali kutekeleza miradi ya maendeleo katika kaunti hizi.
“Rais amewekeza fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo katika kaunti hizi lakini bila kuwepo na amani hayo maendeleo hayataweza kutekelezwa. Kwa hivyo ni jukumu la wakazi wa kaunti hizi kuhakikisha kwamba amani inadumishwa ili kuwe na maendeleo.” Walisema.