SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WAFUGAJI.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na shirika la GIZ inaandaa nakala ya mpango ambao utakuwa ukitumika katika uwekezaji hasa kwenye sekta ya mifugo na maswala ambayo yanapasa kupewa kipau mbele katika kushughulikia maswala ya jamii ya wafugaji.

Akizungumza baada ya kikao na maafisa wa serikali ya kaunti ya Pokot magharibi, afisa kwenye shirika la GIZ Dkt. Oscar Koech alisema kwamba nakala hiyo itatoa mwongozo kwa serikali ya kaunti ya jinsi ya kushughulikia changamoto ambazo zinawakabili wafugaji hasa swala la ukame.

“Tunashirikiana na serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kutengeneza nakala ambayo itatumika kama mwongozo wa kushughulikia changamoto ambazo hasa zinakumba jamii ya wafugaji, zinazotokana mara nyingi na athari za mabadiliko ya tabia nchi.” Alisema Koech.

Aidha Koech alisema kwamba mpango huo unanuia kuwahimiza wafugaji dhidi ya kuhamahama wakitafuta lishe ya mifugo hasa nyakati za kiangazi, ili wawe katika nafasi bora ya kunufaika na miradi ambayo inatekelezwa chini ya shirika hilo.

“Mara nyingi watu ambao tunafanya kazi nao kama wafugaji huwa wanahama kutafuta malisho na maji kufuatia athari za kiangazi, hali ambayo inatupa changamoto ya kutekeleza miradi ya kuwasaidia. Hayo ndiyo baadhi ya maswala ambayo tunajaribu kushughulikia kuhakikisha kwamba hawahami ili wanufaike na miradi hii.” Alisema.

Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya kilimo na unyunyiziaji maji mashamba Peter Kodorang alisema nakala hiyo ni muhimu kwa kaunti hiyo katika kuweka mikakati ya jinsi ya kushughulikia sekta ya ufugaji, na kwamba watahamasisha umma kuihusu punde itakapokamilika.

“Hii nakala itakapokamilika itasaidia kaunti kwa jumla katika kutekeleza mipango yake hasa kuhusu wafugaji. Tutahamasisha jamii kuihusu ili wafahamu kilicho katika nakala hiyo na lengo la kuiandaa.” Alisema Kodorang.